All Sermons
Bible Passage Yohana 8:3-11
This content is part of a series Mahubiri, in .

USIONDOKE NA UPEPO

Date preached June 22, 2025

GLOBAL CHURCH OF CHRIST JESUS TANZANIA
IDARA YA UMISHENI NA ELIMU

Limeandaliwa na Willy Emmanuel

USIONDOKE NA UPEPO
Yohana 8:3-11

3Basi, waalimu wa sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao. 4Kisha wakamwuliza Yesu, ìMwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. 5Katika sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?î 6Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole. 7Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, ìMtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.î 8Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini. 9Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitangulia wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale. 10Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, ìWako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?î 11Huyo mwanamke akamjibu, ìBwana, hakuna hata mmoja!î Naye Yesu akamwambia, ìWala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena

Katika mstari wa 3 tunaambiwa kwamba Waandishi na mafarisayo walimleta mwanamke ìaliyemfumaniwa kwenye uzinziî

Umati huu wa watu baadaye unasemwa kama ìwaoî

Mara nyingi ni ìwaoî ni kweli ni wao!

Huwezi kuwa na mvi bila kukabiliana na mapungufu

Ni heri kuongoza kanisa kuliko kuongoza viongozi

Kadri unavyozeeka inabidi uangalie nyuma.

Inashangaza tunavyowahukumu watu huku tukijitetea wenyewe

Kwenye Saikolojia kuna kitu kinaitwa ìakili ya mkumboî

Ni wakati watu wanapokasirika na watu wengine wanadakia tu na ukweli hauzungumzwi

Ukweli unakuwa lengo baya

Unaona kwenye mitandao ya kijamii, watu wana hasira wakati hata hawajui kwanini wana hasira

Wanapost na kutweet

Jambo linaenea wala hakuna anayefuatilia ukweli

Ni rahisi kudakia na kuwa sehemu ya kundi lenye hasira

Nayasema haya kwa sababu wengi mnadhani ni vigumu kupeperushwa na upepo

Kanisani kwenu kuna mikumbo
Kwenye ukoo kuna mikumbo na shuleni kuna mikumbo

Kama hujiungi na upepo wao wana namna ambayo tunaita ìkukutupia kimvuriî ambapo wanakuwekea wapelelezi wajue kwa nini hujaungana nao

Kwa sababu umekataa kuwa wao

Watakuadhibu kwa sababu tu umeamua ìkufikiriî na kuwa na ìakiliî yako mwenyewe

Wanakuadhibu kwa sababu ya kusubiri ukweli

Hii inatokana na ukweli kwamba wanadamu wanataka kuendana na walio karibu nao

Tunapenda kupenda kupendwa

Utasikia usiposema hivi wewe sio mwenzetu

Wewe sio kanisa letu

Wewe sio kanisa la kweli

Wewe sio familia yetu

Watakwambia hivyo hadi uwe wao

Malcolm Gladwell kwenye kitabu chake kinachoitwa ìmakabilaî amefafanua sana hili

WAMEFUMANIA AKIZINI
Kauli yao tu inaonekana ni waongo
1. Kundi kubwa la Mafarisayo na Waandishi wakubwa na wadogo walitoshaje kwenye chumba ili kumfumania?
2. Kwa nini hawakumleta mwanamume aliyezini naye?
Nafahamu jinsi uzinzi unavyofanywa na jinsi unavyoweza kutambua

Nikawa nawaza wote waliingiaje kwenye chumba hata wote wakawa kauli moja na hukumu inayofanana?

Wanasisitiza kabisa
ìMwalimu! Mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa katika uzinziî

Wanapotaka kujinufaisha kupitia wewe watakuita kwa cheo

Ndani ya heshima unayopewa kuna ndoana

Ndani ya ufadhili unaopewa kuna mtego

Mwanamume aliyezini naye aliachiwa

Nia ya kumleta mwanamke ni kumtega Yesu Kwa hiyo nia hiyo inaweza kutusaidia kwa nini mwanaume hawakuleta

Inawezekanaje watu wawili wanafanya “dhambi” moja lakini anakamatwa mmoja?

Ndiyo maana nawaogopa sana wanadamu

Ni heri niangukie kwenye mikono ya Mungu kuliko kuangukia mikononi mwa wanadamu

Angalau Mungu ana huruma

Wanadamu wakiamua kukupiga mawe inabidi Yesu ainame ndipo utanusurika

Kinyume na hapo watakupiga mawe mpaka upotee

Wanadamu wakisema hawakupendi ni nadra kuona wamebadili walichoamua

Wakati naangalia jinsi mwanamke alivyokuwa anakaribia kupigwa mawe nikawaza kama kulikuwa na mwingine aliyekuwa kwenye hatari ya kupigwa mawe

Ndio, angalia vizuri.

Kila ukiangalia unaona genge kubwa la watu wamejiandaa kuua bila kuwa na ukweli au ushahidi

Jambo gumu kuhusu kuwa kiongozi ni kuwa na ukweli wa unachosimuliwa

Anayekusimulia ndani yake anajitetea

Ukijikuta katika hali hiyo chaguo sahihi ni kunyamaza

Na mkumbo haukusubiri upate ukweli

Kama unasemwa na unajua anayekusema hana ukweli wenyewe na unajua ukitaka kuvunja ukimya unaweza kueleza ukweli

Tatizo ni kwamba utakuwa peke yako na utakuwa unausema ukweli wakati ambao uongo umeingia kwenye damu wamebeba na mawe

Ni lazima ujizuie vya kutosha kulazimisha ukimya

Na kama ukipoteza uadilifu wako ukafungua mdomo unajua mtavuana nguo

Usichukuliwe na mkumbo

Lile genge lilikosea

Sio tu ukweli wa tuhuma bali walikompeleka

Walimpeleka kwa Yesu

Kama walitaka kumuua wangempiga mawe bila kumpelekea kwa Yesu

Wangemuua kule walikomkuta

Lakini ìwaoî Mafarisayo na Waandishi waliungana wakala njama kumleta kwa Yesu
Wanamleta kwa Yesu? Bora wangemleta kanisani

Watu wengi leo hawajui tofauti ya Yesu na kanisani. Wanadhani wokovu upo kanisani

Matendo 2:47

Wanakuja kanisani lakini hamjui Yesu

Wanakuja kanisani lakini hawana uhusiano na Yesu
Hawasemi haleluya kwa sababu wanaelewa bali ni kwasababu kila mtu anasema Haleluya

Na baadaye wanaimba nyimbo za tenzi kama waliookoka

Walimleta Yule mwanamke mbele za Yesu,

5Katika sheria yetu Musa alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?î

Sasa kama sheria ya Musa iliwaamuru je, kwa nini hawajatekeleza? Kwa nini hawajamuua mpaka sasa?

Wanamtumia Yule mwanamke, aidha apigwe mawe au Yesu na Yule mwanamke wapigwe mawe

Hivi unajua watu wanaweza kukuua unapojaribu kufungua mdomo

Naamini kama walimfumania bila shaka hawakumsubiri avae nguo

Kwa hiyo huyu mwanamke yuko mbele za Yesu akiwa uchi, hajavaa nguo vizuri akijaribu kujisitiri kadri alivyoweza

Anajua muda wowote mawe yanaanza kuelea kichwani

Fikiria kupigwa na mawe na unajua kila aliyebeba jiwe alibeba linalotosha kukuua

Fikiria watu wanakutupia mawe, unachanika ngozi, damu zinamwagika kwenye paji la uso

Wengi wanaokuua hawaanzii tumboni kukupiga bali kihwani wanakupiga mpaka unazimia na hawaachi kukupiga mawe hadi unapotea yanaonekana mawe tu

Uzushi ni ni mawe

Uzushi ni mawe na endapo watu wa kutosha watakurushia baada ya muda hutaonekana

Kinachoweza kuonekana ni ìwamewahi kusikia habari zakoî

Kila unapoungana na uzushi unarusha mawe
Wataandikiana meseji kuhusu wewe na atakayepata atafowadi na mwingine atafowad

Kiongozi usichukuliwe na mkumbo, tafuta ukweli

Walimleta kwa Yesu kwa sababu sheria ilimhukumu kwamba apigwe mawe

Kama Yesu akisema ìhapanaî anakuwa hajaheshimu sheria

Kumbuka kipindi hicho bado sheria ilikuwa haijaondolewa

Hapa Mungu anategwa kwa kutumia Mungu

Aliyetoa sheria za Musa ni Mungu na aliyeletewa mwanamke ni Mungu

Huo ndio wakati wa kuongea kidogo na ukimya uwe mwingi na kwa sehemu kubwa ukimya utoshe kuwa jibu refu na maneno yawe jibu fupi

WOKOVU UNAPATIKANA NJIAPANDA NA MAUTI INAPATIKANA NJIAPANDA

Mungu anaokoa anayemchukia. Mungu akimchukia anayemchukia atakuwa amemchukia anayempenda

Yohana 3:16

Shetani alijua Mungu atamchukia anayemchukia lakini alimwokoa Adamu hata kama alichukia alichofanya

Ndio.

Yesu akisema Musa alikosea, wamemnasa

Akikubaliana na Musa, Yule mwanamke anauawa kwa neno lake

Uongozi ndivyo ulivyo

Maamuzi magumu

Unapokutana fikira mbili zinazokinzana

Kila unalowaza kulifanya lina tatizo mbele yake

Unatakiwa kutafuta njia finyu katikati ili unusurike

Uwapishe bila kumuua Yule mwanamke

Walipomuuliza Yesu wewe wasemaje

Alinyamaza

Kisha akainama na kuandika kwa kidole chini

Anafanya alichofanya Baba wakati wa uumbaji Mwanzoni tunamwona Mungu akifanya kila kitu kwa neno
Wanapodhani wamemnasa Yesu kwa mtego wa zamani na Yesu anatumia njia ya zamani kujinasua

Nguvu ya aya haiko kwenye matamshi bali iko kwenye ukimya na kuinama

Ukimya wa mwalimu ni uwezo wa kutofautina na mkumbo

Inabidi unyamaze wakati kundi kubwa linamshambulia mmoja ili ukimya wako uongee zaidi ya maneno yao

Kwa sababu kama ukimya wake una nguvu basi kuinama kwake kuna nguvu zaidi

Aliinama, aliinamia kisichoweza kuinuka wala kujiinua

Kuinama kwake kunaniambia jinsi Mungu alivyonitoa mbali

Niliposhindwa kufika kwake aliinama

Najua umezungukwa na watu watakatifu lakini Mungu anainama kwa ajili ya mwenye dhambi

Ndivyo ulivyookolewa

Anayekubatiza aliinama

Yesu aliinama Wafil. 2:6

Aliinama kutoka kwenye uungu hadi kuzaliwa kwenye hori

Aliinama kutoka kuwa Mungu hadi kuvaa mwili wa udongo

Kuinama ni Injili, Kuinama ni habari njema kwa mwanamke mwenye dhambi

Kwa mlevi, kwa mwizi,

Aliinama kwa ajili yangu

Ndio maana namwinua

Ni lazima niiname ili aniinue

Unapokuwa kwenye matatizo anainama kwa ajili yako

Ulipojaribu kujinyonga, aliinama kwa ajili yako

Ndio maana inabidi umsifu

Ndio maana inabidi umtukuze
Hukuweza kumfikia, yeye alikufikia

Ndio maana Biblia haisemi Mungu alilipenda kanisa bali “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu”

Unaposhindwa kuomba ipasavyo anainama kukusaidia kuomba

Leo atainama kwa ajili yako

Atakuja ulipo ili aitwe imanuel

Ndio maana Yesu aliandika kwenye mchanga

Bila matamshi alihubiri

Bila matamshi alifanya kwa kuinama

Kwa ukimya alikataa kupeperushwa na mkumbo

Alikataa kuungana na mkumbo ili amfunge mwenye dhambi

Kanisa la leo limepoteza injili

Tunaenda kanisani lakini tumepoteza injili

Leo watu wanahubiriwa mafanikio ya nyumba, kuolewa na magari

Zamani watu walihubiriwa kwa sababu Yesu aliinama ili kuwaokoa

Leo watu hawapigi simu ili ukawahubirie, wanapiga simu kwa sababu wanaumwa ukawaombee

Hawahitaji mahubiri yatakayounganisha kwa Yesu na Kanisa bali wanataka maombi yatakawaunganisha kwenye mali na Kanisa

Tumepatwa na nini?

Anapokuwa jela ndio anahitaji maombi kuliko alivyokuwa anaiba

Usipomwamsha mwanao mapema kwenda kusoma, kwenda kufanya kazi

Ataamshwa kwenda kula, kuoga na kulala akiwa kwenye ulimwengu

Takwimu zinaonyesha 70% ya watoto waliokulia kanisani wana nafasi ndogo ya kuwa wakristo ukubwani kwa sababu kama huoni umuhimu wakiwa wadogo utalazimika kukariri Biblia yote wanakuwa watu wazima

Usiangalie wengine wanaleaje watoto

Usiondoke na mkumbo

YESU HAKUVUNJA SHERIA YA MUSA BILA KUIDHINISHA ADHABU YA KIFO

Mathayo 5:17

Kwenye tukio hili alitakiwa aidha avunje sheria ya Musa au aliruhusu huyu mwanamke kuuawa

Angevunja sheria anpigwa mawe yeye

Hakuvunja sheria na wala hakupigwa mawe na tena mwanamke hakupigwa mawe

Alichofanya aliwaongezea uelewa juu ya nafsi zao

Wakati fulani tunatumia maandiko kuwaua watu kiroho wakati na sisi tuna dhambi zilezile

Tofauti yetu na wale tunaowahukumu ni vile dhambi zetu hazionekani.

ìYeye aisye na dhambi awe wa kwanza kutupa jiweî

Ukimzuia wa kwanza umezuia wa pili

Kwenye mstari huu tunaona kwamba hata kama hawakuwa na dhambi maishani mwao lakini njama iliyotengeneza tukio lile iliwaingiza wote kwenye dhambi

Makosa waliyofanya:
1. Walimhukumu bila uhalali Mathayo 18:16 Waliingia moja kwa moja kwenye adhabu Kumbu. 19:15
2. Walimleta ahukumiwe adhabu kwa Yesu wakati kwa Yesu hakuna hukumu ya adhabu Warumi 8:1
3. Wanamleta ambako hakuna adhabu

Najaribu kuwaza kama kulikuwa na ukweli wa tukio lenyewe la uzinzi

Mwizi huja ili kuharibu na kuua lakini Yesu alikuwa kutafuta na kuokoa kilichopotea

Baada ya kuwaambia asiye na dhambi awe wa kwanza kurusha jiwe hakungoja aone mawe na hakungoja majibu bali aliinama

Huyu ndio kiongozi tunayemfuata

Kwa sababu ukipanda mbegu unatakiwa usubiri mbegu iote usiifukuefukue kuona kama inaweka mizizi

Na Biblia inasema:

Wakashitakiwa na dhamiri zao 1 Yohana 3:20; 1 Tim. 4:2

Wakati anaendelea kuandika chini walihukumiwa sio walijihukumu bali walihukumiwa

Walimhukumu mwenye dhambi walihukumiwa na dhamiri zao

Mungu akusaidie uwe na dhamiri iliyo hai isiwe imekufa ganzi

Ruhusa ya kumpiga mawe iliambana na sharti lililowafanya wafikirie

Kwa hiyo awali walimhukumu bila kufikiria kama ni kweli madai ya tuhuma zao

Walimhukumu kwa mkumbo

Kitu kimoja ambacho rafiki na ndugu zako hawataki ufanye ni kutumia kichwa chako

Hawataki utumie akili zako

Mkumbo

Watu wanaochukuliwa na mkumbo ni wale walioshindwa kufikiria

Walimleta mwanamke ahukumiwe na Yesu lakini kumbe walijileta wahukumiwe wenyewe

Kanisa linataka watu walifuate lakini halitaki watu wafikirie

Viongozi wengi hawataki watu wafikirie

Tofauti iliyopo kati ya werevu na wapumbavu ni msitari mwembamba unaoitwa

Kufikiria

Mkumbo unakuzuia kutafakari

Wanataka uwaige lakini hawataki utafakari

Wanataka uwange mkono lakini hawataki utafakari

Ukihoji wanakufukuza, wanakuwekea watu wakupeleleze

Kanisa halipaswi kuwa mkumbo, hampaswi kuchukuliwa na mkumbo

Mkumbo ni upepo, usichuliwe na upepo

Yesu anawapa watu muda wa kutafakari ili waone kama hawana dhambi

Anawapa nafasi hiyo hata wazee (viongozi) waliowazuia vijana kufikiria

Wanaokuzuia kutafakari sio tu wanazuia usitafakari uhalali wa dhambi wanayomshutumu mtu fulani bali wanajua ukitafakari utagundua wanayemhukumu anaonewa na wao ndio wana dhambi walizoficha

-Njia ya kujilinda ni kushambulia

Ndani ya hukumu kuna dhambi ya hakimu

Alipowaambia aanze wa kwanza kutupa jiwe, Walikumkumbuka dhambi zao wakasahau mawe mkononi

Kutafakari kunakusaidia kukumbuka
Anayekuzuia kutafakari anakuzuia kukumbuka

Anakuzuia usiwe na uhusianoo mzuri na Mungu Zaburi 1:1-4

Ndio maana nawaambia wazee kwamba huwezi kuwa na mvi bila kufanya dhambi

Lakini ajabu Biblia inasema;

Waliomleta mwanamke walikuwa wazee na wadogo

Ningetarajia wazee wasitajwe, Nilitarajia vijana wasifundishwe unafiki na kijisahau

Unapofundisha vijana watu kwamba fulani wana dhambi na kesho wanakuta wewe una dhambi ambayo hawakuwahi kuiona wanakuwa wana wa jehanam mara mbili yako

Hapo ndipo watu wa kanisani wananishangaza jinsi wanamvyosahau haraka mtu wanayemwona kwenye kioo

Haki yako isijengwe juu ya huzuni ya watu wengine

Huruma ileile anayohitaji mwenye dhambi unayemhukumu ndiyo huruma ile anayohitaji mwanao

Ni muhimu kuwaelewa watu kwa sababu usichokielewa kina kawaida ya kujirudia

Usiondoke na upepo

Matajiri wana mkumbo

Maskini wana mkumbo

Unakumbuka wale nguruwe 2000?

Ndio, Usichukuliwe na mkumbo, mkumbo ni kundi ulilotoka nalo mbali

Kundi litakupeleka korongoni usipotafakari

Kufuata upepo kutakufanya ufe kabla hujazeeka

Biblia inasema Kundi la nguruwe likatumbukia majini

Kufuata mkumbo kutamaliza maisha yako kabla hayajaanza

Kufuata mkumbo kutakufanya uumize na kuwachukia watu

Kufuata mkumbo kutakufanya ujitenge na watu ambao kiukweli hawana kosa

Yatakupata haya kwa sababu hutaki kutumia nywele zako

DODONDOSHA MAWE ILI MABADILIKO YAJE

Alipoinuka akakuta mawe tu watu wameondoka
Walipodondosha mawe mabadiliko yalianza ndani yao.

Kumuua mwenye dhambi hakuwezi kukuletea mabadiliko (transformation)

Nakupa changamoto hii leo tuone kama unaweza kudondosha mawe uliyokuja nayo bila kuyarusha

Mabadiliko ya nafsi yako hayaanzi kwa kwenda kwenye makongamano makubwa

Hata ukienda kwenye kongamano ambalo walimu ni malaika kama huwezi kuacha kuhukumu wengine huwezi kubadilika

Kanisa haliwezi kubadilika kwa kuitisha mikutano ya Africa, Ya Tanzania nzima

Ya Africa Mashariki n.k

Vijana hawawezi kubadilika hata kama watakusanywa kwenye makambi, kwenye semina za kitaifa na kikanda kama hawawezi kuwaona wazee wao wanajihukumu na kuacha kurusha mawe

Mawe ni uzushi

Mawe ni hukumu ya uongo

Mawe ni majungu

Mawe ni ufarisayo!

Dondosha mawe!

Kila mtu anaweza kukuchoka kama ambavyo unawachoka wengine,

Lakini usipojichoka mwenyewe huwezi kubadilika

Hadi utakaposema sasa basi Luka 15:17-18

KIla mtu alijisemea

ìkama atapigwa kwa mawe sawa lakini sio jiwe languî Kumpiga mawe ni kujipiga mawe mwenyewe kwa kuwa ni dhambi kama yeye japo dhambi yangu haionekani
Natambua kwamba na mimi ni mwanadamu”

 

KANUNI YA KIROHO KWA MTU WA ROHONI:

ìNdugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lolote ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole huku ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na kutimiza sheria ya Kristoî

Yohana 3:16
1Yohana 3:16
Yohana 13:34

Unapomhukumu mtu bila kumrejeza ni uthibitisho tosha kwamba wewe sio mtu wa rohoni

Watu wengine wa namna hii wanatembea na mawe mfukoni, wanangoja wapate mwenye dhambi wayatumia

Wakati fulani unakuwa hujakosea lolote ila kwa vile wanataka kuutumia uzushi kukupaka usoni rangi nyekundu basi watakupaka mpaka hutaonekana kabisa

Wagal. 6 inatufundisha kwamba alighafilika hawi rohoni naye anamhukumu aliyeghafilika hawi mtu wa rohoni Kanisa linakuwa na watu wawili walioghafilika wakati lina mtu mmoja ambaye kanisa limeaminishwa kwamba ana dhambi

Kuna mwingine anakula meza ya Bwana na mwingine inaaminika ametengwa

Kama unajitambua kuwa kiongozi, kama Yesu alivyojitambua utafumba mdomo unaokufanya urushe mawe

Usingoje dhamiri ikufunge mdomo

Watu wenye dhamiri ndio wanaoomba msamaha. Wenye kiburi na kujiona dhamiri zao zilishakufa ganzi. Wanajiona wako mbinguni wakati vichwa viko duniani

Biblia inasema,

Mtu wa rohoni anatakiwa kujiangalia, anatakiwa kujihoji

Anatakiwa kujichunguza

Nilidhani ukiwa mtu wa rohoni huna haja ya kujichunguza, kumbe ukiwa wa rohoni unatakiwa kujichunguza kabla ya kuchunguza

Unatakiwa kujihoji kabla ya kuhoji

Unatakiwa kujiangalia kabla hujaangalia

Fanya hivyo kama kingozi na Mkristo kabla hujawahukumu wengine

Kwa watu rohoni sio kukodolea macho wengine, bali kujiangalia wewe kwanza

Amen!

UMRI HUAMUA MWELEKO MZURI NA MBAYA

ìMmoja mmoja waliondoka kuanzia mkubwa hadi mdogoî

Kuanzia wazee hadi vijana

Tunaonyeshwa hadi umri waliomuhukumu Yule mwanamke

Umri ni uzoefu, umri ni hekima

Walidondosha mawe!

Inamaana waliokuwa mbele na mawe ni vijana, na wazee walikuwa nyuma

Kila anayetumwa anakuwa mbele, anayetumwa hahoji na hatumii akili yake

Vijana walikuwa mbele

Wafadhili walikuwa nyuma

Sijui kama umeokota mawe mwenyewe au umeletewa

Sijui kama umeamua mwenyewe kumchukia mtu au umeshinikizwa lakini nakuona una mawe mkononi

Sijui kwa nini watu wengine huwasalimii wakati hawajakukosea lakini kwa vile wameikosea team yenu

Tunalazimisha rafiki zetu wasiongee na mtu ninawachukia

Iwe kwa akili zako au kwa kuambiwa, unatakiwa kudondosha mawe leo

Wa rohoni hawamhukumu mtu kwa mawe bali kwa upendo

Unajiona una haki kuliko watu wote?

Unajiona unaona una hekima sana? Dondosha mawe bila kurusha

Ukomavu wako haufanani na bei ya mawe uliyoshika, dondosha!

Utumishi wako unalemewa na mawe uliyoshika, dondosha!

Huu sio ujumbe wa kupigiwa vigelegele ni ujumbe wa kujihukumu

Ni ujumbe unatakiwa kukufanya udondoke bila kumrukia mwenye dhambi

Sio kufaidika na upweke wa mtu kwa sababu tu una mawe mkononi

Mawe sio kwa ajili ya watu wa rohoni kuyatumia

Usitumie taarifa ya uongo kuua heshima ya mtu

Usitumie uzushi wa wazushi kuua huduma

Uzushi ni mawe! Dondosha!

 

 

Unatarajiwa kuwa na nguvu ya kutosha kuchukua mzigo wa nduguyo.

” Mchukuliane na kuitimiza sheria ya Kristo.”

Tatizo liliko kati ya mwenye dhambi na waandishi na mafarisayo ni dhambi ya mafarisayo na waandishi

Dondosha mawe!

Unajivuna una nguvu kwenye eneo la udhaifu wa ndugu yako wakati alitakiwa ajione mwenye nguvu eneo la nguvu zako

Lakini una mengi wasiyoyajua watu, ndio maana kwako kudondosha mawe ni vigumu kuliko kuyaweza mfukoni

Mawe hayadondoki kirahisi kwa sababu baadhi yetu tumetoka kwenye familia zinazorusha mawe kirahisi kuliko kudondosha

Mawe hayadondoki kirahisi nyakati ambazo ukweli unafichwa kwa faida ya kumuumiza mtu asiyejitetea

Kinachonishangaza kwenye aya hii ni jinsi walivyoondoka

Waliokuwa nyuma walikuwa wa kwanza kuondoka na waliokuwa mbele walikuwa wa mwisho kuondoka tena mmoja mmoja sio kama kundi

Walipoona wazee wanaondoka na vijana waliondoka

Wazee wanapoondoka hawakukanyaga mawe, vijana wanapoondoka walikanyaga mawe ya wazee

Kumbuka mawe ni majungu, uzushi, uongo, hila na fitina

Vijana wanapaswa kuishi ili waone maisha lakini wametangulizwa kurusha mawe

Wazee hawakujua kuwa kuna gharama ya kujihukumu na kuondoa walichoweka kwenye vichwa vya vijana

Yesu alipoinuka alimuuliza Yule mwanamke

ìwako wapi washitaki wako?î 1 Petro 5:8

Hili ni swali ambalo tunaita rhetorical question

Ni swali ambalo anayeuliza anajua jibu

Ni swali analilohitaji mwenye kuulizwa kuliko jibu analohitaji anayeuliza

Mfano:
Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi?
Tumtii Mungu au mwanadamu?

 

Unadhani Yesu hakujua jibu?

Hata kama aliinama, hata kama hakutumia uwezo wake wa Uungu, lakini angalau alisikia mawe yanadondoka

Lengo la swali lilikuwa ni kumfungua Mwanamke

Kwa wale wanaoongelea mambo yaliyopita miaka 10 iliyopita yameacha makovu ambayo ni hali inayokukandamiza hata huwezi kuinuka kumwangalia Yesu

Msongo wa mawazo unakufanya usiamini kama maadui wameondoka

Unakuwa na msongo wa mawazo unaotokana na ulichofanyiwa miaka 30 iliyopita kana kwamba umefanyiwa leo

Habari mbaya ni kwamba unapumua leo lakini unaishi miaka 30 iliyopita

Habari njema ni kwamba yupo Yesu aliyeinama, na washitaki wako wameondoka,

Kwa hiyo swali la Yesu lililenga kumfanya mwanamke atamke kwa kinywa chake ili afunguliwe Warumi 10:8-10

Haijalishi Yesu alimwaga damu kiasi, usipokiri kwa kinywa chako kwamba hakuna wa kukutenga na Yesu, kila siku utahisi una hatia

Warumi 8:39

Alitaka atamke mwenyewe kwamba wameondoka, hawapo

Huko ndiko kufunguliwa

Kufunguliwa ni kujitambua

Huyu mwanamke amedhalilishwa hadharani, Heshima yake imedhalilishwa

Yesu anamfugua kwenye mateso ya udhalili aliofanyiwa

Haiishi mpaka useme imeisha

Mungu amenituma nikwambia kwamba umefunguliwa, uko huru, ya zamani hayakushikilii. Damu yake ilikufungua

Yeye ambaye mwana amweka huru yu huru kwelikweli

Shetani amechanganyikiwa muda huu kwa sababu alitaka uendelee kugalagala chini

HATUA YA MWISHO YA KUMFUNGUA
Kisha Yesu anasema

ìHata mimi sikuhukumuî
ì Nenda usitende dhambi tenaî

Anaondoka na pengine hakupita njia ileile lakini alirudi kule kule walikomtoa

Safari hii atawakuta bila mawe

Atakuta wamehukumiwa na kufungwa na dhamiri wakati yeye yuko huru

Ili Yesu akwambie sikuhukumu ni lazima useme washitaki hawapo

Kuwa Mkristo sio kuwa maarufu, sio kuwa kundi kubwa

Kundi alilokuja nalo limeondoka naye inabidi aondoke peke yake akiwa angalau amesikia mambo matatu ya kumfungua

1. Washitaki wako wapi
2. Sikuhukumu
3. Nenda usitende dhambi tena

Kama unataka kuwa mtu wa rohoni usiondoke na kundi

Kama unataka kuokoka usiende na kundi

Unapoona umebaki peke yako jua mbele yako yupo Yesu

Unapoondoka, Yesu anabaki na mawe waliyadondosha washitaki

Washitaki walipoondoka waliacha mawe,ili yakukumbushe maumivu ya kudhalilishwa, Usibaki yalipo mawe

Mathayo 11:28-20
1 Pet. 5:6-8 Mwanamke na Yesu

Mwanamke anaondoka anaacha mawe yamebaki na Yesu

Yesu akiondoka anayacha mawe peke yake

Usipokuwa mwangalifu utakuwa kama ìwaoî ìnaoî

Lakini Mungu ameniambia nikwambie

USIONDOKE NA MKUMBO

GLOBAL CHURCH OF CHRIST JESUS TANZANIA
IDARA YA UMISHENI NA ELIMU

Limeandaliwa na Willy Emmanuel

In series Mahubiri