MUZIKI JANGWANI
KUTOKA 15:19-27
Kucheza mziki jangwani. Jangwa na kucheza mziki haionekani kuendana.
Jangwani ni mahali pa kunusurika na sio kucheza mziki. Ni vigumu kuwaona watu wakicheza jangwani lakini wanawake hawa tunawaona wakicheza jangwani.
Katika somo hili nitazungumzia wanawake na Ibada, Wanawake na Neno la Mungu na nitazungumzia maji na mti
Tafakari jambo hili tunapozama kwenye aya hii inayoanza kwa kutuambia wanawake waliocheza kama vile jangwa hawalioni hata kama walikuwa jangwani huku kukiwa na mchanga wenye joto kali nao walicheza kinanda huku Farao akizama na jeshi lake. Walicheza huku maiti za Farasi 600 na wapanda Farasi wake wakielea. Hata kama maiti ziliea hadi ufukweni karibu na walipokuwa lakini waliendelea kucheza muziki. Lazima uendelee kucheza bila kujali ni jangwa gani lipo maishani mwako.
Kwenye maji ndiko tunakokutana na Mungu. Hata mwanzoni tunaona kwamba Roo wa Mungu alitulia juu ya vilindi vya maji. Kuna uhusiano baina ya Mungu na maji; uhusiano ambao ni muhimu sana katika Biblia nzima.
Farao alizama majini, Makuhani kabla ya kuingia patakatifu walinawa kwenye maji, Kizazi kipya kilchozaliwa jangwani kilipita Yordani, Musa alichapa mwamba nao ukatoa maji. Maji yalitoka kwenye mwamba na sio kwenye chemichemi, sio kwenye mto na sio kutoka kwenye korongo bali mwamba ukatoa maji. Sijui ni nini lakini inaonekana Mungu ana uhusiano mkubwa na maji. Yesu alibatizwa kwenye maji na Biblia inasema waziwazi kwamba alipotoka majini mbingu zilimfunukia. Huduma ya Yesu alianza na maji wakati walipoishiwa divai kule Kana aliwaambia wajaze maji kwenye mabalasi na akabadili maji kuwa divai na ndio maana ubatizo ni muhimu sana. Maji yana nguvu, Maji ni alama ya wokovu na maji yana theolojia.
Petro alikutana na Yesu akitembea juu ya maji. Lidia alibatizwa kwenye maji na Towashi alimwambia Filipo tazama maji haya ni nini kinazuia nisibatizwe? Yesu alimwambia yule mwanamke pale kisimani, “ukinya maji nikupayo hutaona kiu tena”
Pia ni lazima ufahamu kwamba mwili wa mwanadamu umeundwa kwa maji. Kwa hiyo mwili sio udongo tu. Mtoto mdogo ana maji 75%,Wanaume wana maji 60%-65%, Wnawake 50%-60%.73% ya Ubongo na moyo ni maji, 63% ya Mapafu ni 63% ni maji, 64% ya Ngozi ni maji, 79% ya misuli na figo ni maji na 31 ya mifupa yako ni maji. Mwili wako umeundwa kwa maji. Unaweza kuishi muda mrefu ukiwa na maji bila chakula kuliko unavyoweza kuishi na chakula bila maji. Mwanadamu ni maji na unahitaji zaidi ambacho ni wewe. Mungu anayapenda maji, Mungu anakupenda.
Mungu alipotaka kuwakomboa wana wa Israeli ni nani angefikiri kwamba Mungu angemuua Farao kwa maji? Mara nyingi hatufikiri kwamba maji ni silaha. Hatuchukulii maji kama zana ya kivita. Kama ningepigana na Farao nisingempiga kwa risasi ya maji lakini Mungu hutumia chochote wala hahitaji bomu na ndio ni hatari kupigana na Mungu. Mapambano yake ni ya kimkakati. Yaweza kuwa chochote kilichoko angani, yaweza kuwa chochote kilichoko ardhini, yaweza kuwa taya la punda. alimuua Farao kwa maji. Maji yaliyomleta duniani ndio yaliyomwondoa duniani. Kuwa makini sana unajikuta adui wa Mungu.
Kama vile Nuhu alivyojenga safina kwa ajili ya mvua ambayo hakuwahi kuiona kabla na mara ikaanza kunyesha kutoka mbinguni na akafungua chemichemi maji ambayo yaliinua safina hadi ikaelea. Viumbe vyote vilivyopona vilipata uzima kwa njia ya maji na kila kilichoangamia kilipata kwa njia ya maji. Je, haikushangazi kuona jinsi Mungu anavyoweza kuleta uzima na mauti kwa njia ya maji muda huo huo. Inategemea ulipo, alikuwa anaangamiza wengine kwa kuwazamisha na kuwaokoa wengine kwa maji yaliyomwinua Nuhu. Maji yale yale huyatumia kutakasa na kubadili
Sio tu aya yetu imejawa na mlio wa kinanda cha wanawake wanaosherehekea uhuru wao lakini pia imebeba mambo matatu ambayo Mungu anataka kutufundisha jinsi anavyotenda kazi penye maji. Ni habari ya wana wa Israeli baada ya miaka 400 ya utumwa. Utumwa wa kimwili kwa kufanyishwa kazi na Wamisri na utumwa wa kiroho kwa kukosa kumwabudu Mungu wao (kutoa sadaka) kwa miaka 400. Kwa miaka mia nne hawakuwa kufanya sadaka za utakaso.
Mtazamo wao juu ya Mungu ulikuwa umenajisiwa na ukaribu wao na Wamisri. Lakini kwa kiasi kidogo walichokumbuka kuhusu Mungu waliomba na kumlilia hivyohivyo. Ninasema mtazamo wao ulinajisika kwa sababu kila wakati walijaribu kujenga sanamu inayofanana na miungu ya Misri. Hata kama nadharia yao ilipotoka lakini sauti ya kilio chao Mungu aliisikia.
ìNimesikia kilio cha watu wanguî
Mungu alisikia kilio cha watu ambao hawakuwa wamemwabudu kwa miaka mingi. Alisikia kilio cha watu waliopotea mwelekeo. Ukungu wa ibada za sanamu na sanamu za miungu ulitanda katika fahamu zao. Ilipita miaka 400 tangu walipomtumikia lakini alikisikia kilio chao. Naweza kutulia hapa hapa na kusema, ìAsante Mungu kwa kusikia kilio changeî
Daudi alisema nampenda BWANA kwakuwa anasikia kilio changeÖ.Zaburi 116:1-2
Sijamtumikia wala kumtolea sadaka kiasi cha kutosha kujibiwa. Lakini ìnampenda BWANA kwakuwa anaisikiliza sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake; Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote. Kadri niwapo hai na taabu kuinuka nitamshikilia yeye tu. Mpende Mungu ajibuye kili chao walioanguka. Walikuwa wametengwa na Mungu wao kwa miaka yote hiyo na kujikuta wamenaswa kwenye mtego wa utumwa. Hata hivyo, walipomlilia Mungu aliwasikia, Mungu wangu! NI reheme kiasi gani kwamba Mungu anasikia kilio cha mwanawe amabaye hajatoa sadaka na wala kumtumiakia kwa miaka 400 kiasi hata cha kupigana kwa ajili yao? Kwamba Mungu atapigana kwa ajili ya kundi la watumwa? Hata hivyo Mungu aliingia vitani kwa ajili yao kana kwamba walikuwa watakatifu. Watumwa walikuwa ni bidhaa ya kununua na kuuzwa, zawadi ya kupeana harusini na hata hivyo Mungu alimwambia Farao;
ìIsraeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wangu wa kwanza wanguî Kutoka 4:22
Usipomwachia mwanangu, nitawaua wanao. Usipowatoa watu wangu nitapigana nawe kwa sababu nimesikia kilio chao hata kama ni wapotevu, nimesikia kilio chao.
Kuna hali humtokea mzazi anaposikia kilio cha mwanawe. Kuna kilio mtoto anaweza kulia kila mtu akaendelea kuangalia TV lakini kuna kilio cha mtoto mzazi akikisikia anaweza kudondosha glasi na kila baba atadondosha jembe. Kuna ukaribu Fulani ambao ukisikia mtoto wako analia unabadilika. Unakuwa na nguvu ya ajabu kuliko ulivyokuwa kabla ya kusikia kilio. Ni hali aliyoiweka Mungu kati ya mzazi na mtoto. Mungu anasema nimesikia kilio cha watoto wangu, nitapigana nawe kwa zana ambazo hujawahi kupigwa nazo. Nitakupiga kwa inzi, Nitakupiga kwa vyura, nitakupiga kwa nzige, nitakupiga kwa maji.Kwa hiyo Mungu aliingilia kati na kuandaa mpango wa kuwatoa baada ya hiari kushindikana.
Siku zote Mungu ana mpango wa kukutoa kwenye taabu yako. Kama utabaki taabuni basi ni wewe mwenyewe unakuwa umeamua kubaki
Kabla kuzimu haijakuuliza swali Mungu analo jibu.
ìJaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lile lililo kawaida ya binadamu lakini pamoja na lile jaribu aliweka mlango wa kutokeaî 1Kor. 10:13
Katika aya yetu tunaona Mungu alivyo na mikakati kwa sababu kwanza anawataka Waisraeli wapake damu ya kondoo kwenye miimo ya milango yao ili mauti isiwapate. Mungu alipoona damu Waisraeli hawakuhitaji hifadhi, alipoona damu hawakuhitaji hema. Hawakuhitaji silaha, hawakuhitaji dawa; hivi unaye Mungu aliyekuruka ulipopaswa kufa. Mauti ilikuruka! Ungekuwa umeshakatiliwa mbali lakini alikuruka, ungekuwa umeshaangamia, ungemezwa mzima mzima lakin alifanya njia ya mauti kukuruka. Kwa ajili ya hiyo,hata asiponipa chochote nitamsifu tu, hata asiponipa nilichomwomba leo nitamwinua. Simwabudu kwa sababu ya familia aliyonipa, simwabudu kwa sababu ya nyumba, la, bali namwabudu na kumtumikia kwa sababu mauti imeniruka.
Hivyo ndivyo watu wa Mungu walikuwa zamani. Siku hizi tuna kanisa ambalo linamsifu Mungu kwa sababu ya mali, kwa sababu ya mafanikio, kwa sababu ya maduka, kwa sabau ya mchumba, kwa sababu ya kazi. Watu wa Mungu walimsifu Mungu zamani kwa sababa Mungu alichovya mavazi yao kwenye damu ya mwanakondoo, walimsifu Mungu kwa sababu maiti ya Farao, wapanda farasi na Farasi zinaelea baharini. Sifa za namna hii hazisikiki sana siku hizi
MISRI KAMA DOLA KUU
Kitu unachotakiwa kuelewa ni kwamba wakati Waisraeli wanatolewa Misri, nchi ya Misri ilikuwa dola kuu. Ilikuwa juu ya falme zote. Farao wa Misri alikuwa ni kiongozi ambaye akiamua ufe unakufa. Akiamua unaweza usipumue tena. Alifanya maamuzi vijiji vilichomwa moto. Ndiyo maana Musa alikimbia na kukaa midiani miaka 40. Ni aina hiyo ya Farao ndiye aliyekuwa anawakimbilia Waisraeli kabla hawajavuka bahari. Hivi, unaweza kufikiria hofu kiasi gani iliwapata waliposikia vishindi vya farasi mia sita nyuma yao. Sio tu farasi bali farasi maalumu wa kivita wenye kasi, wenye nguvu na askari weredi wa kivita akiwafukuzia watumwa na wakulima wa Gosheni bondeni pembezoni mwa Bahari ya Shamu. Na kama Mungu asingefanya njia wangeangamizwa kabisa. Maana Daudi anatukumbusha;
ìKama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa, Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, wanadamu walipotushambulia..î Zaburi 124:1-2 SUV.
Msomaji, kama Mungu asifanya njia ungeangamizwa kabisa. Mwanadamu hawezi kukusaidia, mjomba hawezi kukusaidia, Marafiki hawawezi kukusadia, Majirani wameshindwa kukusaidia uko katika hali ambayo lililo mbele yako linakutisha kama walio nyuma yako lakini Mungu akiwa upande wako ni zaidi ya ulimwengu ulio dhidi yako. Mungu amekusudia kukutoa, amekusudia kukunyakua akupeleke mbali na hofu, mbali na wasiwasi. Najua unasikia vishindo vya mafanikio ya watesi, unasikia vishindo vya vitisho vya maadui wala usihangaike maana ni kawaida adui kukutisha kabla hajakuangamiza. Adui anataka utishike na kuogopa ili kazi ya kukuangamiza iwe nyepesi
Hili halikuwa shambulio la kuvizia. Waisraeli waliweza kusikia kishindi cha miguu ya matatizo nyuma yao. Hisia zao ziliganda, utashi wao ukapooza. Wakashikwa na mfadhaiko, wakaanza kunungíunika na kulalamika dhidi ya Mungu na Musa. Hii ni kawaida, adui anapokutisha anataka uwashambulie ulio jirani nao, uwaone wao ndio chanzi cha yanayokupata kisha kila mtu atakuacha na ndipo adui atakushambulia. Wanatishwa na Wamisri lakini wanagombana na Musa na Mungu. Wakataka kurudi Misri japo sijui kama Farao alienda kuwachukua ili warudi Misri au angewaua. Wanaona bora kufia Misri, wanaona bora kurudi utumwan. Kila unatamani mabaya kuliko mema inakuwa ni kwa sababu ya hofu. Lakini leo ni siku yako ya kufunguliwa.
Biblia inasema Mungu alitumia kilichokuwa mkononi mwa Musa kupamabana na kile kilichokuwa mkononi mwa Farao. Farao alikuwa na magari ya Farasi 600, wapiganai hodari lakini Mungu alikuwa na upepo na maji. Mugu aliposema na upepo, upepo ukavuma na kuyasukuma maji na kuyagawa iliapatikane njia ya Waisraeli kupita. Sio tu aliwavusha bahari ya shamu bali aliwavusha kwa raha. Upande wa pili wa tukio hili ni kwamba kugawanyika kwa bahari ya shamu Mungu anawafundisha Waisraeli nini maana ya kutengana.
Mungu aliwatenganisha
Ni Mungu wa kutenganisha, ndiye alitenganisha mchana na usiku, alitenganisha nuru na giza. Alitenganisha maji ya ardhini na maji ya angani. Na Mungu anatumia maji kuwafundisha kwamba atawatenganisha na Farao kwa maji na Upepo uliovuma ni Roho Mtakatifu. Tazama uhusiano wa Roho Mtakatifu na upepo Mwanzo 1:1-3; Matendo 2:1-4 kisha soma na Yohana 3:5
Neno la Mungu linasema walipokanyaga ardhi iliyokuwa chini ya bahari ilikuwa kavu. Mungu anapokutoa kwenye utumwa atakupitisha katika mlango ambao hutapata matope maana baadaye sana Paulo anasema ule ulikuwa ndio ubatizo wao. Kwa kuwa ndivyo, basi katika ubatizo ni lazima farao wako awe amekufa lakini ukivuka naye atakutesa.
Muda mwingi sikujua kwamba Waisraeli walikuwa wanapewa huduma ya ubatizo. Kutenganishwa na Farao. Hata waisraeli walidhani wanatoka utumwani lakini Mungu anasema haikuwa kutoka tu bali ilikuwa ni ubatizo wa ondoleo la Misri. Waliingia baharini wakiwa watumwa watoro lakini walipotoka majini walikuwa Taifa la Mungu. Ilikuwa lazima wabatizwe ili kutofautisha utambulisho wao wa kwanza na utambulisho baada ya kutoka majini na hiyo ndiyo kazi ya ubatizo
Warumi 6:3-4
Waliingia majini ili adui aliyekuwa anawakimbilia atangazwe amekufa, Ili utu unaokimbiliwa na Farao ufie majini, Utumwa ufie majini. Tulikufa majini kama watumwa lakini tulitoka majini kama Taifa huru wakati Farao anaendelea kutafuta alichombilia baharini nacho ni mauti yake mwenyewe na mauti ya watumwa wake na aliokuwa nao.Maana Farao aliingiza mguu kupita kwenye njia ambayo Mungu aliifanya kwa ajili ya watu wake badala ya kuwa njia ambayo hata adui anaweza kupita, Mungu aliuambia upepo urudishe maji nao wakazama. Ndiposa najua kwa hakika Mungu ndiye Bwana wa upepo! Anaweza kuukemea ili utulie na kuuruhusu uvume kwenye maisha yako ili kukuokoa na kuwazamisha maadui.
Magari 600, Farasi 600, askari 600 wakiwa mapanga, wakiwa wanazama ngao zilikuwa zinaelea juu ya maji. Mwanahistoria Josephus anasimulia kwamba miili ya Farasi, askari, na Farao ilielea hadi ufukweni mwa bahari. Kwa hiyo unapoona Biblia inasema wanawake walimsifu Mungu, walimsifu huku maiti wanaziona na usidhani Farao alizama bila kujaribu kuogelea ili kujiokoa. Ni nani alidhani kwamba Mungu atakuokoa ili ucheze mbele ya maiti ya dhambi zilizokutesa? Mbele ya maiti ya hila za watesi? Ndiyo maana unatakiwa kumsifu Mungu jangwani kuliko utakavyomsifu ukiwa kwenye nchi ya ahadi kwa sababu ukicheza jangwani utakuwa unacheza huku Ibilisi anaangamia. Unapomsifu Mungu jangwani magonjwa yako yanakufa, unapokuwa jangwani maadui wanakufa. Jangwa ni Kanisa la Wairaeli lakini pia jangwa ni maisha ya majaribu na taabu. Katika maisha yote haya tunatarajiwa kuwa na furaha
Miriamu alipochukua kinubi mkononi mwake sio kwa sababu ya furaha tu bali ya vitani. Unapoona Mungu amekutoa usimame tu na kumwangalia bali furahia. Ukimsifu Mungu nyumbani kwako, katika sebule yako ni maji yanatitika kumwangamiza adui Yohana 7. Kuna mambo maishani mwako hayawezi kutokea hadi utakapofunua kinywa chako. Kataa kusononeshwa
Wamisri waliofuatia wana wa Israeli walizama wote hakuna aliyesalimika. Mauti kwa adui ilikuwa ni 100% hakuna aliyesalimika ili akatoe taarifa kwao. Mungu anaposema nitawaangamiza adui zako mbele ya macho yako anamaanisha kuwaangamiza 100% haijalishi adui ni mkubwa kiasi gani Mungu atamshusha chini.
Bahari ilijirudi sio tu Farao aangamie bali ili Waisraeli watapofika katikati ya jangwa wasiweze kurejea Misri kwa njia ile. Uambie moyo wako ìsiwezi kurudi tena maana niko mbali sanaî. Hii ndiyo maana ya kutengana ambayo Mungu anayotaka tuijue.
Maji machungu (Uchungu maishani mwetu)
Aya yetu inazidi kutumbia kwamba kulikuwa na safari ya siku tatu jangwani ndipo wakafika mahali penye maji na walipojaribu kuyanywa maji yalikuwa machungu. Haina maana kwamba yalikuwa mabaya; na watu wakalia. Mara zote watu wanapomlilia kiongozi ni kana kwamba kiongozi alikuwa na maji ya kunywa ambayoo sio machungu, kiongozi anaduwaa. Lakini sio tu walimlilia Musa bali walilia dhidi ya Musa. Na kitu pekee kama kiongozi watu wanalia dhidi yako ni kumlilia Mungu. Musa akamgeukia Mungu. Kazi mtumishi wa Mungu ni kupeleka kwa Mungu kilio cha watu na kuwambia watu maagizo ya Mungu
Msalaba tiba ya uchungu
Walimlilia Musa juu ya maji na Musa alimwambia Mungu kuhusu maji lakini Mungu alijibu kwa mti. Umeomba hili na Mungu anakupa lile. Jibu la Mungu halilingani na ombi. Umepiga magoti unaomba kwa ajili ya maji lakini anakupa mti. Huu ni wakati pekee wa utakaso. Huu ni wakati ambao sio tu Mungu anataka kujibu haja yao bali anataka kuwakutanisha na msalaba wa Kristo. Ni kama anawaonyesha msalaba lakini kwa mbali.
ìUkinywa maji nikupayo hutaona kiu tenaî Yohana 4
Kama ukiendelea kunywamaji unayokunywa utaona kiu tena, utaendelea kwenda kuchota maji. Kuna tatizo kwenye maji unayokunywa lakini ukimywa maji nikupayo hutaona kiu tena. Waliomba maji akawapa mti. Mti ni Kalvari. Mti ni msalaba. Msalaba ndio njia pekee aliyonayo Mungu ili kuyafanya maji ya maisha yako yawe matamu. Mungu alimwambia Musa, najua tatizo ni maji lakin jibu ni mti! Mungu wangu! Tatizo lako linaweza kufanana na mti lakini suluhisho lako ni mti. Jibu haliendani na ombi lakin Mungu alimwambia Musa atupe mti kwenye maji. Mtembelee mpendwa mwambie tupia mti kwenye tatizo lako. Najua unahitaji pesa lakin tupia msalaba, najua unaomba maji lakini tupia mti. Mti uligeuza maji machungu ya Mara kuwa matamu. Ile kuhusishwa mti maji yalibadilika. Matamshi yako yamekuwa machungu mno, maisha yako yamekuwa machungu! Tupia msalaba kla mtu atatamani kukusikiliza. Mungu atageuza giza maishani mwako kuwa nuru. Suluhisho la maji machungu lilikuwa palepale.
Warumi 10:8-10
Yesu aliyebadili maji machungu kuwa matamu ndiye aliyebadili maji kuwa divai. Jibu la yote ni msalaba. Golgotha uliinuliwa msalaba ulionivuta. Nauenzi msalaba uliobadili machungu yangu kuwa utamu. Haijalishi umekuwa na uchungu wa madawa ya kulevya, uchungu wa kufanyiwa ukatili, uchungu wa kubakwa. Sijui ni uchungu gani ulionao hata Waisraeli walikuwa na uchungu wa kutumikishwa na kunyanyaswa na uchungu wa maisha yao waliukuta kwenye maji. Mti uliyafanya maji kuwa matamu waliutupa mti kwenye nayo yakabadilika.
Mara ni mahali pa utakaso. Ni mahali ambapo uchafu unaonaodolewa. Uchungu wa Misri unaondolewa. Hivi, unajua maisha yako yanahitaji nini sasa hivi? Yanahitaji mti. Huhitaji gawio ila mti, huhitaji mapato bali mti. Una sura nzuri lakini unahiti mti. Una nywele nzuri lakini unahitaji mti. Una taaluma lakin unahitaji mti. Maisha yako na ulimi wako bado vina ladha chungu kwa sababu hujatupia mti. Msalaba Pekee ndio unaweza kubadili maji machungu kuwa matamu. Kila kilicho kichungu kilimezwa na mti.
Yohana 1:39 ìTazama mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu.î
Rudia kusoma Yohana 7
Aliondoa kila laana na manuizi! Aliondoa lilisimama kinyume change aliondoa, Kila pepo lililosimama kinyume change aliondoa. Alimeza! Alifanyika dhambi kwa ajili yangu. Alifanyika uchungu kwa ajili yangu. Kwa ajili ya makosa yangu alichubuliwa. Aliumizwa kwa ajili yangu. Kwa mapigo yake naliponywa (Isaya 53). Msalabani alimeza uchungu wangu wote. Yeyey asiyejua dhambi akafanyika dhambi ili niwe na haki mbele za Mungu kama vile sijawahi kuwa mchungu. Aliubadili uchungu wangu wangu kuwa utamu kwa sababu ya mti.
Baada ya muujiza songa mbele;
Baada ya kunywa maji na kutosheka hatupaswi kubaki tuatangatanga kwenye muujiza. Tatizo la Kanisa la leo ni kwamba tumejenga makumbusho na kuningíiniza vichwa vyetu juu ya mambo ambayo tunapaswa kuyaacha na kusonga mbele hati kufikia kimo cha ukuaji. Kubadili maji machungu kuwa matamu Mungu hakumaanisha waendelee kukaa hapohapo. Hata kama ni matamu walilazimika kusonga mbele.Hawakutakiwa kutengeneza mafundisho na kuwa mwongozo bali Mungu alikuwa na mengi mengine mbele yao na njia pekee ya kuyaona mengi ilikuwa ni kusonga mbele
Visima 12 na mitende 70
Kutoka 1:1-4
Matunzo endelevu
Tumetoka kwenye hatua ya kutenganishwa, tukaingina katika hatua ya utakaso na sasa ni hatua ya matunzo endelevu kwa sababu makabila yako 12 yaliyotokana na watu 70 walioingia Misri. Ni matunzo aliyowaandalia Mungu kabla hajawatoa Misri. Yupo aliyechimba visima hivi lakini kwanini achimbe 12 na apande mitende 70. Inaaminika kwamba mtu anaweza kuishi muda mrefu sana akila tende na kunywa maji bila kula chakula kingine. Ndiyo maana nakwambia Elim ni alama ya matunzo ya kudumu. Ni nani anajua kama hawakuchuma na tende wakiwa Elim? Kuna mtu alichimba visima hivi ili Waisraeli wakifika wakute visima viko tayari.
Walipokunywa maji ya Mara hawakujenga hema pale lakini walipofika kwenye visima vya Elim walipiga kambi. Mungu atakupa Baraka za matunzo an sio ya muda mfupi.
Jangwani kulikuwa na visima vya maji na mitende kwa ajili ya watu wa Mungu. Visima vimechimbwa tayari cha kufanya ni kuchota na kunywa, unatakiwani kupiga kambi tu huku kimvuri kikiwa ni mitende.
Mungu aliwapa pumziko.
Mathayo 11:28-29
Mungu mwenyewe alikuwa wingu mchana na nguzo ya moto usiku lakini hapa aliwapa mitende wakae chini ya kimvuri chake. Mungu anakaribia kukupa kimvuri. Umepita kwenye majira ya moto uchomao lakini Mungu amekuandalia mitende. Wakati mti mwingine ulitupwa kwenye maji lakini mitende ilifanyika kimvuri. Tunaendelea kuona miti na maji na Mungu anataka kufundisha kitu kuhusiana na majina miti. Je, unahitaji kimvuri? Umekuwa ukitembea kwenye majira ya jua kali? Waliketi kimvurini, wakapumzika jangwani. Nakutamkia pumziko maishani mwako. Mungu akufikishe kwenye pumziko. Miti ya mitende imeandaliwa kwa ajili yako na visima vimechimbwa tayari. Umejitaabisha kuchimba visima kwa nguvu zako miaka hii yote lakini safari hii Mungu amekuandalia. Mungu amewaandalia pumziko Waisraeli katika taabu ya mtu mwingine. Unajiuliza nitalipataje pumziko hilo? Utalipata kwa kujua kumsifu Mungu jangwani
Kadri unavyoendelea kunungíunika na kulalamika hutaweza kuona mitende yako lakini utakapoamua kujitambua na kuinuka kumsifu Mungu utauona utukufu wa Mungu. Nami nitamwabudu Mungu katikati ya jangwa langu. Mungu atanitoa kwenye hofu, atwapiga adu zangu na kunipa pumziko. Nitatakiwa kufanya muda huu ni kusherehekea katikati ya jangwa maana katikati ya majanga na ukame wa uchumi ndipo mtu Fulani ananichimbia visima name nitayanywa maji yake.
Ewe mtu wa Mungu furahi kwa sababu kwa sasa anayetakiwa kughadhibika ni Ibilisi. Kama hukuzama Bahari ya shamu unapaswa kufurahi kwa sababu Mungu amevunja uti wa mgongo wa laana na ameondoa kumbukumbu mbaya za laana ya woga ili usiishi maisha yote kama kmkimbizi. Ndio maana Miriam aliimba na kucheza. Wanawake walicheza si tu kwa sababu Farao na jeshi lake wanazama bali kwa sababu watoto wao watakaozaliwa hawatazaliwa utumwani tena lakini ilionyesha mzigo walioishi nao muda mrefu, mzigo wa shauku ya ushindi. Mungu atafuta kumbukumbu zote zinazokutesa. Atakuandalia visima na mitende na kama umesimama katika imani jangwani mwimbie Mungu sasa. Ndiye avunjaye kongwa lililowekwa shingoni mwako na jana yako. Utakuwa mwingine kabisa. Utapitia majaribu mengi lakini hutarudi Misri. Utapata upinzani mkali lakini hutakuwa mtumwa wa Farao unayemwona leo. Ndiyo Miriam alicheza!
Alicheza kwa sababu alijua ndugu zake hawatafyatua tofali za mapiramidi tena. Alicheza kwa sababu ya kesho inayongíaa. Tuwapate wapi wanawake kama huyu?
Ewe mwanamke! Mwambie shetani, ìhutampata mwanangu, hutawapata wajukuu zangu na vitukuu vyangu. Cheza jangwani hadi nira zikatike. Mungu anataka umsifu mitaani hadi watu waone jinsi unavyofurahi jangwani japo walitarajia jangwa litakudhalilisha. Paza sauti sauti kama tarumbeta; mwimbie Bwana kwa sauti ya ushindi majumbani mwenu. Hujafika hapo ulipo ili uiname. Hujafika hapo ulipo ili ugande.
Wafilipi 4:4-6
Ukimpa Mungu sadaka ya sifa atakupa maji na kumaliza kiu kabisa. Ninakutangazia majira mapya maishani mwako. Nakutangazia maji katika jangwa lako. Chemichemi zitaibuka kila upande.
Kama hujampokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yako wasiliana nasi kwa huduma ya mafundisho zaidi
1. Utapata nafasi ya kusikia neno la Mungu na sio muhubiri Warumi 10:17
2. Utapata nafasi ya kutafakari na kuliokea neno kwa imani Waebrania 11:1,6; Yakobo 1:26; Matendo 2;41
3. Itakuwa ndio njia pekee na fursa ya kubadili njia na kumgeukia Mungu Matendo 26:18-19; 17:30; 3:19-22
4. Mabadiliko yako yatakuwa ushuhuda wenye kumkiri Mungu na Yesu Kristo Mathayo 10:32-33; Wafil. 2:6-10
5. Kisha utahitimisha kwa kubatizwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi Matendo 22:16; 16:30-34; 2:37-42; Marko 16:15-20
6. Baada ya hapo utatarajiwa kuishi maisha ya ushindi na ushuhuda
Mungu yupo tayari kutupa mti katika maisha yako. Kama unaamini Injili lakini hujawahi kubatizwa na umekuwa ukikimbizwa na maisha yako ya nyuma, unatakiwa utafute mto na kushuka majini kama Lidia, Kama towashi alivyofanya Matendo 8:26-38; 16:14-15. Fanya kama Kristo alivyofanya na akama Waebrania walivyofanya
Sasa nataka niombe na wewe;
ìBaba katika jina la Yesu tunaomba maji ulituwekea. Hata ikiwa kwa kutambaa tutambaa ili tuyapate, Ikiwa ni kwa kulia, tutalia tutalia ili tuyapate. Bwana turejeshee furaha, lirejeshe Kanisa lenye kujawa na sifa zako. Tunanyenyekea Bwana, tunaima. Hatutaondoka katika jangwa hili bila kukusifu. Haijalishi itachukua muda mrefu kiasi gani nitaipambania sifa na furaha mchana na usku. Nitaomba alfajili, nitaomba adhuhuri nitaomba lichwapo.
Nitasimama leo nikusifu daima. Mbingu na zitabasamu kwa ajili ya makuu uliyonitendeaî
Endelea kuomba hadi maji yabubujike ndani yako, Omba hadi chemichemi zitokee, Omba hadi kukutane na miti ya mitende
Kwa jina la Yesu Kristo, Amen!